Saturday, March 10, 2018

KIJANA NA HAMASA: UMUHIMU WA NIDHAMU YA PESA



Sio swala la kushangaza mtu kumiliki pesa na kuishiwa pesa. Unaweza kujiuliza kwanini watu wanapata pesa lakini kwa muda mfupi wanaishiwa? Pesa imekuwa changamoto sana kwa watu wengi hadi imefikia hatua watu wanasema pesa ni mashetani, mara wanasema pesa zina wenyewe. Jibu ni hapana Pesa sio mashetani wala hazina wenyewe ila ni jinsi gani unakuwa na nidhamu punde unavyokuwa na hiyo pesa.
Unaweza kujiuliza Nidhamu ya pesa ni nini? Nidhamu ya pesa ni pale unapokuwa na uwezo wa kuicontrol pesa na kuweza kufanya kazi zako kwa mipangilio bila ya kuja kujutia kwa badae. Mara nyingi sana watu wanashindwa kujizuia pindi wanapokuwa na pesa sababu ya kukoswa nidhamu ya pesa.
Namna gani unaweza kuwa na nidhamu ya pesa?
Ndugu, sizani kama hapo ulipo hujawahi kumiliki kiasi cha pesa Fulani hapo nyuma. Hebu jaribu kuchukua hata muda wa dakika mbili ujiulize hiyo pesa uliifanyia matumizi sawasawa na ambayo unafikiria ungefanya kama ungekuwa nayo hiyo  pesa.
Usijilaumu sana kwa matumizi hayo ya pesa yaweza kuwa labda usingefanya hivyo usingefikia hapo ulipo haijalishi ni maisha mazuri au duni. Sasa hebu tuangalie ni jinsi gani unaweza kuicontrol fedha na ukafanya vitu ambavyo hutakuja kujutia baadaye.
Kwanza Jifunze kuweka bajeti. Wengi wetu tunapata pesa na kuanza kufanya matumizi bila hata ya kubajeti pesa iliyopo sababu kubwa inayopelekea watu wengi kutumia pesa hovyo mwisho wa siku baada ya pesa kuisha ndio anakumbuka kufanya bajeti hewa yaani mtu anakumbuka kufanya mipango baada ya pesa kumuishia.
Pili Panga manunuzi yako Kabla. Ni jambo la hekima na busara kupangilia kile unachotakiwa kununua maana hili nalo limekuwa tatizo kubwa linalowakumba watu mfano mtu anakwenda sokoni kununua nguo anafika huko anaongezea manunuzi ambayo hata alikuwa hajapangilia halafu mwisho wa siku anaanza kujilaumu.
Tatu Tumia kidogo kuliko Unachokipata.Hapa ndio kuna shida kubwa sana watu wanashindwa kusimamia mapato na matumizi na katika vitu viwili ambavyo vinafanya mtu aendelee na asiendelee ni mapato na matumizi maana watu wengi wanakuwa na matumizi ambayo yanazidi kipato kitu ambacho kinarudisha  nyuma maendeleo.
Nne Jifunze kuweka rekodi ya matumizi yako. Kitu kinachoweza kusaidia sana katika kuweka nidhamu ya pesa zako ni kurekodi ya matumizi unayofanya hii itakusaidia kutathimini kiasi cha mapato na matumizi kwa muda mwafaka na hivyo kukufanya  utambue kama unafanya maendeleo au laa.
Hizo ni baadhi ya njia zitakazo kufanya ujue nidhamu ya pesa.hivyo unaweza kuona ni umuhimu gani unaoweza kuupata juu ya nidhamu ya pesa  .Katika siku ya leo napenda nikwambie kitu kimoja. Pesa siyo kila kitu katika dunia hii lakini ina nafasi kubwa sana. Hivyo ukitaka kuwa na utawala mzuri katika maisha yako ni vyema ukaimarisha misingi ya matumizi ya pesa yako. Epuka tabia za kitoto au za watu wasio kuwa na busara, ambao hula na kutumia kila wanachokipata Naamini njia hizi zitakupa mwanzo mzuri wa matumizi ya pesa zako.

1 comment:

  1. Pesa sio kila kitu katika dunia hii lakini ina nafasi kubwa sana.

    ReplyDelete