Sunday, October 21, 2018

UMEJITOA?



Hakika penye nia pana njia , ni tumaini langu tumekuwa tukinufaika sana na mafundisho haya ya Timiza ndoto napenda kukukaribisha sana wewe msomaji kama ni mara ya kwanza basi tumekuwa na makala mbalimbali ambazo zimekuwa zikifafanua kwa undani na jinsi gani tunaweza kufanya ili kuweza kufikia ndoto zetu ambazo zimekuwa ni kitendawili kisichokuwa na jibu katika maisha yetu haya. Naomba twende pamoja katika makala ya leo ya UMEJITOA? 

Ili ufanikiwe kwa kiwango kikubwa sana ni muhimu sana kujitoa katika maisha yako. Kwa leo napenda nizungumzie hili neno kujitoa kwa namna nyingine kidogo. Watu tumekuwa tukipambana na kuwa na jitihada kubwa sana katika maisha yetu lakini bado kuna vitu tumekuwa tukivishikilia ambavyo kwa namna moja au nyingine vimekuwa ni kikwazo katika kufikia ndoto zetu. Ninaposema kujitoa naamanisha ni muhimu uache kufanya vitu Fulani ambavyo unavipenda sana kuvifanya ila vinakurudisha nyuma ama havina mchango wowote katika maendeleo yako.
Kuna vitu vingi sana ambavyo unapenda kuvifanya na unavifurahia. Ila kwa kuendelea kufanya vitu hivyo inakuwa ni vigumu sana kwako kuwa tajiri. Ni muhimu ujue vitu hivyo na kuviacha mara moja ili uweze kufanya vile vitakavyokufikisha kwenye ndoto zako. Kwa mfano kama unapenda kutumia fedha kwenye starehe kwa kiwango kikubwa inakubidi upunguze sana au uache kabisa starehe hizo ili utumie fedha zako vizuri kuwekeza na utumie muda uliokuwa unaupoteza kwenye starehe kujifunza zaidi kuhusu kazi au biashara zako. Unaweza fikiri kuacha starehe ni jambo la kawaida tu  ni lazima ujitoe maana kama kitu umekizoea  ni vigumu sana kusema  kuanzia sasa unaachana nacho na ukaacha kweli.

NI NAMNA GANI TUNAWEZA KUJITOA?
Ili uweze kufikia ndoto zako kweli ni lazima ujitoe. Kuna vitu ambavyo inabidi uache kuvifanya au kujihusisha navyo mara moja ili uweze kupata muda zaidi wa kufikiria malengo na ndoto zako.
Najua mpaka sasa umeshaweka malengo na mipango itakayokufikisha kwenye ndoto zako na pia umeshapanga matumizi mazuri ya muda wako pengine tayari umeshaandika vitu vyote unavyotamani kuwa navyo kwa baadae sasa ili kujitoa naomba ufanye hivi;
Chukua kalamu na karatasi ama notebook na uandike vitu vyote unavyofanya na muda wako kuanzia muda unaoamka mpaka muda unaorudi kulala ukijumlisha na muda wa kulala. Fikiria kwa wiki chache zilizopita vitu ambavyo umekuwa unafanya kila siku. Baasa ya kuandika vitu hivyo angalia ni vitu gani vinachukua muda wako mwingi na umuhimu wake kwenye malengo ya kutimiza ndoto zako. Kama vitu hivyo havina mchango kwenye malengo yako viache mara moja. Vitu kama kwenda baa kila siku, kuangalia tv zaidi ya masaa mawili kwa siku, kupiga hadithi zisizo na msaada kwako na mabishano yasiyo ya msingi unatakiwa uviache mara moja. Kama unalala zaidi ya masaa nane pia unapoteza muda hivyo punguza muda wa kulala uwe nane au saba kwa siku.
Chukua kalamu na karatasi tena na uandike vitu vyote ambavyo vinatumia fedha zako. Andika vitu vyote ambavyo vinatumia fedha zako. Andika vitu vyote ambavyo unanunua kila siku, wiki na hata mwezi. Kisha angalia ni vitu gani ambavyo sio muhimu sana kwenye malengo yako na maisha yako uvitoe kabisa. Matumizi yote ya fedha ambayo ni ya anasa unaweza kuyatoa kwa sasa unapotengeneza njia za kutimiza ndoto zako.
Kitu chochote ambacho unapenda sana kukifanya ila hakina msaada wowote kwako kufikia malengo ya kuwa tajiri inabidi uache kuvifanya mara moja ili uanze kufanya vile vitakavyokufikisha kwenye ndoto zako.
Ahsante sana kwa siku ya leo napenda nikukaribishe katika makala nyingine inayofuata ikielezea kwa undani MTAZAMO WAKO NI UPI KUHUSU MAISHA YAKO. 

Friday, October 19, 2018

UNAMFANYIA KAZI  NANI?


Habari tena ndugu, ni tumaini langu tena hujambo na unaendelea vizuri. Karibu kwenye mwendelezo wa makala ambazo nimekuwa nikizitoa katika blogu na app ya Timiza ndoto. Ndugu kabla sijaendelea kufafanua zaidi kuhusu kichwa tajwa hapo juu napenda nikusihi kitu kimoja  “ Ubora wa mwalimu darasani unaonekana zaidi pale wanafunzi wake wanapofaulu kwenye mtihani wala siyo darasani tu namna gani anafundisha”  kwahiyo itakuwa haina maana ya kuendelea kufuatilia blogu na app Timiza ndoto kama utaishia kusoma tu bila kuchukua hatua sitahiki katika maisha yako. Naomba twende wote hatua kwa hatua ahsante.
Mpaka sasa unamfanyia kazi nani? Ni kichwa cha makala chenye swali ambalo linahoji kuhusu kazi yako. Hebu tafakari.
Unafanya kazi kukuza mradi wako au unafanya kazi ya kukuza miradi ya watu wengine? Napenda niseme kitu kimoja cha msingi sana hakika kama unamfanyia mtu mwingine kazi nafasi ya kutimiza wewe ndoto zako ni ndogo sana.  Naamanisha kama mpaka sasa umeajiriwa na huna mawazo ya kutoka kwenye ajira yako kuna uwezekanao mkubwa sana wa kusikia tu neon kutimiza ndoto.
Sisemi kwamba ajira ni mbaya au kwenye ajira huwezi fikia ndoto zako. Hebu tuangalie hali halisi, kama umeajiriwa angalia sehemu yako ya ajira ni watu gani ambao wanalipwa fedha nyingi kiasi cha kuwafanya wapate utajiri? Utakuta ni wachache sana , tena ni wakurugenzi na mameneja wakubwa. Nyie wafanyakazi wengine wa kawaida mishahara haikutani , yaani mshahara wa mwezi huu unaisha kabla ya kupata mshahara wa mwezi unaokuja. Hebu tuangalie nafasi ya wewe kufikia kiwango hicho cha ukurugenzi au umeneja! Ni nafasi ndogo sana kwako wewe kupata cheo hicho kwa sababu kipo kimoja tu na wenye sifa wanaweza kuwa wengi. Ndio maana nasema nafasi ya wewe kufikia malengo yako kwa kumfanyia mtu mwingine kazi yaani kuajiriwa ni ndogo sana.
Kama umeajiriwa hata ukafanya kazi kwa kiwango kikubwa kiasi gani bado mshahara wako utakuwa uleule ama utaongezeka kidogo sana. Wakati mwingine unaweza kupewa pongezi kidogo ambayo hailingani na jitihada zako. Ila kama unafanya kazi yako mwenyewe iwe umejiajiri au biashara jinsi ambavyo utaongeza jitihada ndivyo utavyozidi kuongeza kipato chako. Hakuna wa kukupangia kiwango cha kipato ila wewe mwenyewe.
TUFANYE NINI KUFIKIA MALENGO YETU?
Kama tayari upo kwenye ajira anza kufanya mipango ya kujiajiri ama kufungua biashara baadae. Kama bado hujaingia kwenye ajira weka mipango ya kutoingia kabisa au panga kuingia kwenye ajira na kukaa muda mfupi tu ili kupata uzoefu na mtandao na baadae uondoke ukafanye kazi zako. Usisubiri kukaa  kwenye ajira mpaka utakapostaafishwa utashindwa kutimiza malengo yako na ndoto zako.
Ukikaa sana kwenye ajira unajisahau na unakuwa unawaza matatizo tu unayokutana nayo kwenye ajira yako na jinsi mshahara ulivyo kidogo na matumizi makubwa. Hebu kwa mara moja acha kufikiria matatizo hayo ya ajira na ufikiri ni jinsi gani utaondoka kwenye matatizo hayo. Weka mipango ni lini utaondoka na utakwenda kufanya nini?.
Tunaishi kwenye kipindi ambacho tuna fursa nyingi sana za kutengeneza kipato ukiacha ajira. Angalia ni fursa ipi inayokufaa wewe kisha uanze kujifunza vitu vya msingi kuhusiana na fursa hiyo. Kikubwa tumia ujuzi ulio nao, tumia uwezo mkubwa ulio ndani yako pamoja na vipaji vya kipekee ulivyo navyo na angalia mazingira yanayokuzunguka ili uone ni kitu gani cha tofauti unaweza kufanya.
Kwa kujiajiri au kufanya biashara unatengeneza uhuru zaidi wa kuweza kupata kipato kinacholingana na jitihada zako. Pia unaweza kuwasaidia watu wengi zaidi kwa kutengeneza ajira.
Ni katika mwendelezo wa makala zinazopatikana katika blogi na app ya Timiza ndoto karibu tena kwa makala ijayo UMEJITOA?  

Tuesday, October 16, 2018

NGUVU YA WATU UNAOISHI NAO



Ndugu, karibu tena katika mwendelezo wa makala ambazo zimekuwa zikitolewa katika blogu na app ya timiza ndoto ni tumaini langu unaendelea vizuri na kunufaika na mafunzo haya ambayo kimsingi ukisoma na kuyachukulia hatua ni ngazi pekee ya kukufanya ufikie malengo yako na kutimiza ndoto zako.
Leo naenda kuzungumzia swala la msingi sana ambalo linaweza kukufanya ufikie malengo yako au usifikie malengo yako na kutimiza ndoto zako. NGUVU YA WATU UNAOISHI NAO.
Watu unaoishi nao ni kipimo tosha cha kukutambulisha kama unaweza kufikia ndoto zako au la. Kuna msemo wa waswahili ambao unasema  Ndege wanaofanana huruka pamoja ” kwahiyo kupitia watu unaoishi nao tunapata picha nzima ya maisha yako maana mawazo na mtazamo mzima wa watu mnaoishi nao ni lazima ufanane. Kama umezungukwa na watu ambao ni maskini na wana mawazo ya kimaskini hakuna njia yeyote unayoweza kukwepa umaskini kama utaendelea kuwa nao.

Watu ulioko nao karibu kama ndugu, jamaa, marafiki na hata wafanyakazi wenza wana ushawishi mkubwa sana kwako. Unaweza kuwa na mawazo mazuri sana ya kuondoka kwenye umaskini wako ila unapowapa mawazo yako watu wako wa karibu kama wana mawazo ya kimaskini watakuwa wa kwanza kukukatisha tamaa. Ni rahisi sana kuwasikiliza kwa sababu huenda unawaamini sana na pia upo karibu nao sana hivyo unashindwa kuwapinga. Kwa njia hii unajikuta unaendelea kuwa maskini licha ya jitihada nyingi unazofanya za kujikwamua kwenye umaskini huo.

Jaribu kuchunguza vizuri na kwa makini uangalie mfumo wako wa maisha na vitu unavyofanya havitofautiani sana na vile wanavyofanya watu unaoishi nao kwa muda mwingi. Wote ni kama mna mfumo mmoja wa maisha utakuta wote mmeajiriwa au mnafanya biashara , mkitoka kazini labda jioni mnakutana baa kupumzika, hadithi zenu zinahusisha mambo mengine tofauti tu. Kwa njia hii unajikuta wote mna uchumi unaofanana. Kama watu unaoishi nao muda mwingi hawana ndoto kubwa kwenye maisha yao watakuzuia na wewe kuwa na ndoto kubwa. Kama watu hao hawaoni umuhimu wa kubadili maisha yao, watakuambukiza na wewe tabia hiyo.

Sasa ufanye nini kama umeshagundua kwamba watu unaoishi nao wanakuzuia kufikia malengo na ndoto zako. Naomba fanya mambo matatu yafuatayo;

  1.   Punguza muda unaotumia kukaa na watu hao. Jinsi ambavyo unatumia muda mwingi na watu hao ndivyo unazidi kupokea sumu zao. Hivyo kuwa makini na punguza muda unaotumia kukaa na watu hawa , pia angalia ni mambo gani ambayo unaweza kuwashirikisha . kama watu hawa wamekuwa kikwazo kwako kufikia malengo na ndoto zako kwa kukukatisha tamaa acha kuwashirikisha mawazo yako makubwa. Anza kubadili maisha yako taratibu bila ya kuangalia wao wanafanya au kusema nini.
  2. Anza kutafuta watu ambao wana mawazo makubwa na wenye mafanikio ndo utumie muda mwingi kuwa nao. Kwa kukaa na watu wa aina hii utaanza kuambukizwa tabia zao ambazo zimewafanya wakaendelea. Kwa kusikiliza maongezi yao na kuona mitazamo yao inakuwa rahisi sana kwako kubadili mtazamo wako. Kwa kuwashirikisha watu hawa mipango yako mikubwa watakupa moyo uifanye kwani wengi wao walishapita kwenye hiyo na wanajua inawezekana.
  3. Kuwa na mshauri mzuri. Mara nyingine ni vizuri kuwa na mshauri ambaye mnakuwa mnakutana kila baada ya muda unamweleza umefikia wapi na changamoto unazokutana nazo na mshauri huyo anakuwa anakufuatilia na kukusaidia jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali unazokutana nazo. Ni vyema mshauri wako awe ni mtu ambaye ameshafanikiwa kwenye hicho unachotaka kufanya. Isiwe unafanya biashara halafu mshauri wako ni mtu ambaye siye mfanyabiashara. Mtu wa aina hii hana msaada mkubwa kwako kwa sababu hajui nadharia ya kile unachokifanya.


Kwa njia yoyote utakayotumia kujiondoa kwenye umasikini hakikisha umezungukwa na watu ambao wana mawazo kama ya kwako na wanaelekea unakoelekea kwa kukaa na watu ambao hawana mpango na maisha yao watakunyonya nguvu yote na mabadiliko yaliyo ndani yako. Ahsante sana kuwa kuwa nami naomba tukutane tena kwa makala ijayo.UNAFANYA KAZI NA NANI?

Saturday, October 13, 2018

USIKUBALI KUSHINDWA.



Kufeli katika mipango au mikakati uliyojiwekea ni kitu ambacho kinatokea kwa kila mtu. Na ni wakati ambao mtu anakuwa njia panda katika kufanya maamuzi ama kuendelea au kuacha.
Wakati unapopitia hatua hii katika mipango yako huu sio wakati wa kuruhusu na kukufanya wewe uweze kukata tamaa katika safari yako badala yake unatakiwa upanue ufahamu wako ujue ni namna gani ya kuendelea na kukufanya ufike pale ulipotaka kufika.
Ndugu napenda kukuambia kitu cha msingi sana ambacho unatakiwa kukifanya endapo utaanza kuona dalili za kufeli katika mipango yako, kwanza unatakiwa ujue kwamba hutakiwi kujiona kama wewe ni mkamilifu kwa kitu ambacho unakifanya (do not need to be perfect or perfectly extraordinary just be better version of you

Mara nyingi tumekuwa tukiangalia hasa mabadiliko ya vitu tunavyovifanya tukisahau kuangalia mipangilio yetu ikoje na inaendeleaje? Kufanya kazi kwa muda mrefu bila kuona mabadiliko hakumanishi kama mipango yako imekufa au laa , hapo kinachotakiwa na kusubiriwa ni wewe kujua unatakiwa upangilie kwa namna gani ili uweze kuona mabadiliko unayoyataka. Mwandishi mmoja aliandika  “When you have a day when you fall down on the diet, instead of telling yourself that you are weak or bad, tell yourself that you had a bad day and that tommorrow’s a new day to start is over.”

Ni muhimu sana kuwa mstahimilivu , kuwa na upeo wa kutambua kitu mapema itakusaidia sana kusonga mbele katika safari yako halafu tambua ni rahisi sana kukata tamaa kuliko kujipa moyo hivyo badala ya kuruhusu mawazo hasi yanayokujia kwenye ufahamu wako ni muda sasa wa kuwa na mawazo chanya na kuondoa yote mawazo mawazo ambayo yatakupelekea kukata tamaa katika kufikia ndoto zako.

Tuesday, October 9, 2018

AINA AU KOO ZA KUKU;



Koo za kuku zinazopatikana hapa Tanzania; kuna koo nyingi za kuku zinazopatikana hapa nchini;
Baadhi ya koo  hizo na sifa zake ni hizi zifuatazo;-
1.    KUCHI
Sifa zake za kuchi;
a)      Ana umbo lenye ukubwa wa wastani.
b)      Hana upanga kichwani.
c)      Ana mdomo mfupi.
d)      Ana shingo ndefu yenye manyoya.
e)      Ana ngozi ya rangi ya njano.
f)       Ana miguu mirefu isiyo kuwa na manyoya.
g)      Ana uwezo mkubwa wa kujihami.
h)      Wanapatikana mikoa ya Tabora , Singida , Shinyanga , Mwanza , na Tanga.
2.    KISHINGO
Sifa zake za kishingo;
a)      Ana umbo lenye ukubwa wa wastani.
b)      Ana upanga kichwani.
c)      Ana shingo isiyo na manyoya.
d)      Ana ngozi yenye rangi ya njano au nyeusi.
e)      Ana miguu mifupi isiyo kuwa na manyoya.
f)       Anapatikana mikoa yote Tanzania.
3.    BUKINI
Sifa zake za bukini;
a)      Ana umbo fupi na ni mnene.
b)      Ana upanga kichwani.
c)      Ana shingo yenye manyoya.
d)      Ana ngozi yenye rangi ya njano.
e)      Hana manyoya ya mkia.
f)       Wanapatikana kwa wingi katika mikoa ya Tanga , Pwani , Kilimanjaro , na Singida.
g)      Ana miguu mifupi isiyo kuwa na manyoya.
4.    KINYAVU AU NUNGUNUNGU AU KUCHERE.
Sifa zake kinyavu;
a)      Ana umbo dogo ukilinganisha na kishingo na kuchi.
b)      Ana shingo yenye manyoya.
c)      Ana ngozi yenye rangi ya njano.
d)      Ana manyoya yaliyosimama.
e)      Ana mkia mrefu wa wastani.
f)       Ana mkia mrefu wa wastani.
g)      Anapatikana katika mikoa yote nchini.
5.    KAWAIDA UA KITEWE.
Sifa zake kitewe;
a)      Ana umbo dogo ukilinganisha na kuchi na kishingo.
b)      Ana shingo yenye manyoya.
c)      Ana ngozi yenye rangi nyeupe njano na nyeus.
d)      Ana manyoya ya mkia yenye urefu wa wastani.
e)      Anapatikana mikoa yote ya Tanzania.
Ndugu, tambua unapofanya kitu ukiwa unakijua vizuri ni hakika  utafanya kwa ufanisi zaidi ukilinganisha na kama hujui. Ni fursa yako sasa kuchagua ni kuku wa aina gani unaweza kujikita kufuga kwa maendeleo yako katika eneo ulilopo ahsante sana kwa leo naomba tukutane kwenye makala ya LISHE YA KUKU NA KUCHANGANYA CHAKULA.