Thursday, March 22, 2018

KIJANA NA HAMASA: SIRI KUBWA YA MAFANIKIO.

Ni siku nyingine tena tukiendelea na mfululizo wa makala hizi kwa undani zaidi siri ya kupata pesa (Utajiri) na kuendelea kuwa na pesa (Utajiri).
Watu wengi wamekuwa wakizunguka huku na huko wakitafuta hasa nini siri ya utajiri na wengine hadi kukimbilia imani potofu ili mradi tu wapate mali (Utajiri). Ni njia gani rahisi ambayo inaweza kuleta mafanikio kwa uharaka hili limekuwa ni swali ambalo linatawala vichwa vya wengi.
Na kitu kinachoponza zaidi ni pale mtu anapohitaji mafanikio kwa  urahisi na kwa haraka zaidi. Ndugu leo napenda nikupe siri moja tu ya mafanikio ambayo inaweza kuwa njia ya pekee ya kukuvusha daraja katika maisha yako.
Mafanikio hayatafutwi kwa dawa au zile imani potofu wanavyodai wengi. Mafanikio yanakuja pale mtu unapotambua anataka nini katika maisha yake. Maana yake kwanza anatakiwa atambue kwanini anataka utajiri au mafanikio? Halafu baada ya hapo akishapata sababu za kwanini anataka kuwa tajiri atafute sasa ni njia gani au namna jinsi afanye ili aweze kujikwamua sehemu alipo siyo kutafuta njia rahisi tu na ya haraka.
Watu wengi wamekuwa wakihoji na kuuliza kwa watu waliofanikiwa katika maisha yao kwamba ni njia gani wametumia hadi kufanikiwa? Jibu la moja kwa moja hapo ni kwamba huwezi ukajua ni njia gani zinazomfanya mtu afanikiwe kama hujajua kwanini unataka ufanikiwe katika maisha yako?. Maana mfano mzuri ni kwamba wengi husingizia tatizo ni mtaji lakini ni wangapi ambao wanakuwa na pesa za kuanzisha kitu chochote lakini anakaa muda mfupi tu anakuwa hana kila kitu kwahiyo ndugu kama hujajua kwanini unataka kuwa na mafanikio huwezi ukajua ni njia gani za kukufanya uwe na mafanikio.
Katika siku ya leo naomba uchukue tathimini dogo na ya haraka katika maisha yako Ni kweli katika maisha yako hujawahi kupata pesa ambayo kwa leo unafikiria ingekuwa mtaji kwako? Au Ni fursa ngapi umezipata hapo nyuma ambazo unafikiria ungekuwa nazo leo ungekuwa umejikwamua na maisha yako? Ndugu ukipata majibu ya maswali hayo naamini utakuwa umenielewa na kuelewa hasa nini siri kubwa ya mafanikio?
Sipo hapa kukukatisha tama maana unajua ni wapi ulipita lakini cha msingi hebu tafakari sasa kwa makini halafu ufanye yafuatayo;
1.       Acha kuendelea kuongea tu (Stop talking) najua una mipango mingi sana lakini cha kukushauri hebu acha kuishia kuwaza na kuongea tu na kuendelea  kupanga kila siku.
2.       Toa ndoto zisizo na kikomo (Stop dreaming) hizo ndoto ulizonazo haziwezi kutimia kwa kuwa nazo bila utekelezaji.
3.       Chukua hatua madhubuti ( Start Commiting) huu ni wakati wako kuanza kutekeleza kile unachokihitaji katika maisha yako acha woga mawazo yako ni sahihi hebu jaribu kutembea na hisia zako ili uweze kufanikiwa katika maisha yako.
Ndugu nashukuru sana kwa siku yako kuweza kufuatilia  huku nikiamini umenielewa na hili litakuwa ni chachu kubwa ya mafanikio yako ahsante sana kwa muda wako kwa siku ya leo naomba tukutane tena kwa makala zijazo ili tuendelee kujifunza zaidi kuhusu maisha yetu ni ukutakie uwe na siku njema

Tuesday, March 13, 2018

KIJANA NA HAMASA: NGUVU YA MAWAZO YAKO.

Ndugu, Mpendwa ni tumaini langu wewe ni mzima wa afya tele. Itakuwa ni jambo njema ukichukua muda hata wa dakika moja uweze kumshukuru Mungu kwa hii nafasi uliyoipata siku ya leo. Maana kuna ambao walitamani kuiona siku hii lakini haikuwezekana.
Katika siku ya leo napenda nifungue ukurasa mpya ambao umekuwa ni changamoto kwa watu wengi sana wakiumiza vichwa ni namna gani ya kupata pesa(Utajiri) na kuendelea kuwa nayo siku zote.
Hebu tuweze kuangalia kwa undani ni namna gani NGUVU YA MAWAZO YAKO inaweza kukufanya upate pesa, halafu uendelee kukaa na pesa siku zote. Imefikia hatua hadi watu wanafanyiwa tunguli kwa sababu ya kulinda pesa zao lakini napenda nikuibie siri nzito sana leo.
Katika vitu vyenye nguvu na ambavyo vinafanya mtu afanikiwe ni uwezo wa akili yako (Power of your Mind), Tatizo linakuja pale Nguvu na Uwezo wa akili yako inapofanya kazi katika upande sahihi au usio sahihi. Mwandishi mmoja wa Kitabu aliandika (“One big difference between the rich and the poor is that poor people says “I can’t afford it;” more often than rich”) “Tofauti kubwa kati ya mtu tajiri na Mtu maskini ni Kwamba Maskini husema “Siwezi kufanya hiki” Tofauti na watu matajiri halafu akaendelea kusema (“Poor people use poor words and poor words create poor people means Your words do become flesh”) “Watu  maskini hutumia maneno ya kimaskini na maneno ya kimaskini hutengeneza watu maskini” na maneno yako waswahili wanasema Maneno huumba.
Katika ukurasa huu, ndugu naomba ujifunze tofauti ya maneno ya tajiri na maneno ya maskini , maneno yenye kasi kubwa na maneno yenye kasi ndogo na katika hili utatambua ni namna gani unaweza kubadilisha maisha yako kwa kutumia maneno yako na jinsi gani unavyofikiria na kama utaweza kubadili maneno yako na mawazo yako kama matajiri, ukawa na mawazo chanya  naamini ukipata pesa , utaendelea kuwa na pesa kwa urahisi sana
Ahsante sana kwa siku ya leo naomba tukutane kwenye makala ijayo .

Monday, March 12, 2018

KIJANA NA HAMASA: NGUVU YA MAARIFA

Ndugu, Tupo kwenye dunia iliyojaa maarifa ya kila aina na kila kukicha vitu vipya vinabuniwa  ili kusaidia watu kufanya mambo yao kwa urahisi na kwa muda husika ni wakati wako sasa kufikiria ufanye nini ili uweze kwenda jinsi dunia inavyokwenda.
Maarifa ni njia inayotumiwa kujitoa katika shida.Maarifa ni njia ya kupata kitu.Maarifa ni Elimu au ujuzi ambao anaupata mtu ili uweze kumsaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
Watu wengi wanatafuta elimu ili iwasaidie kupata kazi; hayo ni makosa makubwa. Unachopaswa kutafuta ni MAARIFA ili yakusaidie kupata kazi ya kufanya.
Wengi husema Pesa ni kila kitu katika dunia hii. Sio kweli lakini naweza kusema Pesa ina nafasi kubwa sana katika dunia lakini cha muhimu katika vyote hivyo ni MAARIFA maana naamini ukiwa na maarifa unaweza kuwa na chochote unachokitaka. Katika siku ya leo napenda tuangalie ni nini hasa nguvu ya maarifa na inakusaidiaje katika mambo yako.
VITABU ni nguvu kubwa sana ya maarifa ambayo inafanya watu wazidi kuwa wabunifu kila kukicha lakini changamoto kubwa ipo kwa Waafrika maana hadi siku umekuwepo msemo unaosema Ukitaka umfiche Mwaafrika kitu cha thamani Kiandike kwenye Kitabu
Mpendwa leo napenda kukuhamasisha tu ya kwamba ukitaka kufanikiwa na kuendelea kwa kasi ya 4g ni kusoma Vitabu maana katika vitabu unaweza kujizolea faida nyingi sana kama ifuatavyo;
Ubunifu watu wengi sana wamekuwa wabunifu na kuzidi kugundua mambo mapya sababu ya kusoma vitabu ambavyo vinawafanya kuwa welevu na kupata maarifa mbalimbali ambayo wanapoyatumia katika hisia chanya yanawaletea maendeleo makubwa sana katika maisha yao na jamii inayowazunguka.
Uhamasikaji ,Tupo kwenye dunia ambayo imejaa vikwazo na vigingi vingi sana watu wamekuwa wakikatishana tamaa sababu ya kukoswa maarifa ndugu ukiwa una nasoma vitabu utahamasika na kupata nguvu ya kufanya mambo makubwa ambayo hata ulikuwa hutarajii kufanya katika maisha yako.
Kutunza muda wako ndugu naamini unapokuwa unatenga muda wa kusoma vitabu itakufanya kuwa makini na muda wako na kujijengea tabia ya kujisomea, moja kwa moja unaanza kujijengea tabia ya kutunza muda. Hutapoteza tu muda na kuona huna cha kufanya kwa sababu muda wote una kitabu cha kusoma. Na pale ambapo una kitu cha kukusukuma umalize kitabu haraka kila dakika chache utakazopata utazitumia vizuri kusoma
Kuongeza Kipato chako Unapokuwa msomaji wa vitabu naamini utakuwa mbunifu , utahamasika ,utaweza kutunza muda wako kitu ambacho kitakuwezesha kuongeza kipato chako katika kitu chochote unachokifanya
Kuna faida nyingi sana unaweza kupata kupitia kusoma vitabu ndugu kama hujaanza au huna pa kuanzia naomba unitafute kwa namba na email iliyopo hapo chini niweze kukupa mwanga zaidi ni nini ufanye ili tuweze kwenda sawasawa na dunia yetu hii iliyojaa maarifa na ubunifu wa kila kukicha sio mwingine ni mimi muhamasishaji wako Yohana Shigukulu ahsante sana kwa muda wako kuutumia na kuweza kusoma makala hii naomba tukutane kwa makala zijazo.


Sunday, March 11, 2018

KIJANA NA HAMASA: UKWELI KUHUSU NDOTO ZAKO

Ndoto ni kitu ambacho mtu hutamani kuwa na malengo ambayo kila mtu anawaza kufikia na kutimiza katika maisha yake. Japo kila mtu ana ndoto zake tofautitofauti, Changamoto inakuja kwenye kutimiza ndoto zake. Sio siri watu wamekuwa na ndoto ambazo siku zote hazitimii kwa sababu mbalimbali hadi kusababisha  kuwa na imani potofu na kujisema  Mungu hajampangia kufikia pale anapopahitaji kufika.Wapo watu wamekuwa na ndoto mbalimbali kama kuwa Profesa , Daktari ,Engineer, Mfanyabiashara n.k lakini mwisho wa siku anajikuta tofauti na alivyokuwa anawaza. Imekuwa changamoto kubwa inayosumbua watu wengi katika kutimiza ndoto. Mfano mzuri ni wewe hapo hivi kazi hiyo uliyonayo au kitu hicho unachofanya ndio zilikuwa ndoto zako tokea mwanzo?
Katika makala hii napenda nikushirikishe ni nini kwa sasa unaweza kufanya ili uweze kufanikisha ndoto zako. Naamini kama utafanya sawasawa na inavyotakiwa haitachukua muda kutimiza ndoto zako naomba uangalie kanuni ifuatayo ili uweze kutimiza ndoto zako.
MIPANGO +VITENDO ==>DARAJA==> NDOTO ZAKO
PLANS + ACTIONS==>BRIDGE ==>DREAMS
Najua una ndoto ambayo unayo na unatamani siku moja uitimize. Cha kufanya hebu kaa chini utafakari kwanza hiyo ndoto yako mfano una ndoto za kuwa mfanyabiashara mkubwa wa kitu Fulani .Kabla ya kufanya kitu chochote,
Kwanza Andaa Mpango mkakati unaohusu hiyo ndoto yako upangilie ni wapi uanzie na wapi uelekee na siri moja kubwa katika mipango yako ni kuwa na Imani na hicho unachokifanya naamini ukiseti mipango yako sawasawa itakuwa ni moja ya hatua katika kutimiza ndoto zako.
Pili ukishakamilisha mipango yako anza kufanyia Vitendo vile vyote unavyovipanga ukifuata hatua moja hadi hatua nyingine na kwa kufanya hivyo Mpango mkakati + na Vitendo itakuwa ni Daraja la Kutimiza Ndoto zako.
Ndugu, Tupo kwenye dunia iliyojaa maarifa ya kila aina na kila kukicha vitu vipya vinabuniwa  ili kusaidia watu kufanya mambo yao kwa urahisi na kwa muda husika ni wakati wako sasa kufikiria ufanye nini ili uweze kwenda jinsi dunia inavyokwenda.kwa maelezo zaidi juu ya chochote unachoweza au unatamani ufanye unaweza kunitafuta kupitia whatsap no.iliyopo hapo chini. Ahsante sana kwa muda tukutane tena katika makala zijazo kwa kutambua na kuelewa maarifa zaidi.

Saturday, March 10, 2018

KIJANA NA HAMASA: UMUHIMU WA NIDHAMU YA PESA


Sio swala la kushangaza mtu kumiliki pesa na kuishiwa pesa. Unaweza kujiuliza kwanini watu wanapata pesa lakini kwa muda mfupi wanaishiwa? Pesa imekuwa changamoto sana kwa watu wengi hadi imefikia hatua watu wanasema pesa ni mashetani, mara wanasema pesa zina wenyewe. Jibu ni hapana Pesa sio mashetani wala hazina wenyewe ila ni jinsi gani unakuwa na nidhamu punde unavyokuwa na hiyo pesa.
Unaweza kujiuliza Nidhamu ya pesa ni nini? Nidhamu ya pesa ni pale unapokuwa na uwezo wa kuicontrol pesa na kuweza kufanya kazi zako kwa mipangilio bila ya kuja kujutia kwa badae. Mara nyingi sana watu wanashindwa kujizuia pindi wanapokuwa na pesa sababu ya kukoswa nidhamu ya pesa.
Namna gani unaweza kuwa na nidhamu ya pesa?
Ndugu, sizani kama hapo ulipo hujawahi kumiliki kiasi cha pesa Fulani hapo nyuma. Hebu jaribu kuchukua hata muda wa dakika mbili ujiulize hiyo pesa uliifanyia matumizi sawasawa na ambayo unafikiria ungefanya kama ungekuwa nayo hiyo  pesa.
Usijilaumu sana kwa matumizi hayo ya pesa yaweza kuwa labda usingefanya hivyo usingefikia hapo ulipo haijalishi ni maisha mazuri au duni. Sasa hebu tuangalie ni jinsi gani unaweza kuicontrol fedha na ukafanya vitu ambavyo hutakuja kujutia baadaye.
Kwanza Jifunze kuweka bajeti. Wengi wetu tunapata pesa na kuanza kufanya matumizi bila hata ya kubajeti pesa iliyopo sababu kubwa inayopelekea watu wengi kutumia pesa hovyo mwisho wa siku baada ya pesa kuisha ndio anakumbuka kufanya bajeti hewa yaani mtu anakumbuka kufanya mipango baada ya pesa kumuishia.
Pili Panga manunuzi yako Kabla. Ni jambo la hekima na busara kupangilia kile unachotakiwa kununua maana hili nalo limekuwa tatizo kubwa linalowakumba watu mfano mtu anakwenda sokoni kununua nguo anafika huko anaongezea manunuzi ambayo hata alikuwa hajapangilia halafu mwisho wa siku anaanza kujilaumu.
Tatu Tumia kidogo kuliko Unachokipata.Hapa ndio kuna shida kubwa sana watu wanashindwa kusimamia mapato na matumizi na katika vitu viwili ambavyo vinafanya mtu aendelee na asiendelee ni mapato na matumizi maana watu wengi wanakuwa na matumizi ambayo yanazidi kipato kitu ambacho kinarudisha  nyuma maendeleo.
Nne Jifunze kuweka rekodi ya matumizi yako. Kitu kinachoweza kusaidia sana katika kuweka nidhamu ya pesa zako ni kurekodi ya matumizi unayofanya hii itakusaidia kutathimini kiasi cha mapato na matumizi kwa muda mwafaka na hivyo kukufanya  utambue kama unafanya maendeleo au laa.
Hizo ni baadhi ya njia zitakazo kufanya ujue nidhamu ya pesa.hivyo unaweza kuona ni umuhimu gani unaoweza kuupata juu ya nidhamu ya pesa  .Katika siku ya leo napenda nikwambie kitu kimoja. Pesa siyo kila kitu katika dunia hii lakini ina nafasi kubwa sana. Hivyo ukitaka kuwa na utawala mzuri katika maisha yako ni vyema ukaimarisha misingi ya matumizi ya pesa yako. Epuka tabia za kitoto au za watu wasio kuwa na busara, ambao hula na kutumia kila wanachokipata Naamini njia hizi zitakupa mwanzo mzuri wa matumizi ya pesa zako.

Friday, March 9, 2018

KIJANA NA HAMASA: WOGA NYUMBA YA UMASKINI.




Kilio ,Ni kilio kila kukicha afadhali ya jana. Limekuwa ni janga kati ya majanga yanayosumbua barani Afrika yakiwemo Vita , Maradhi n.k
 Umaskini umekuwa ni tatizo la kukaliwa kila leo kutafuta ufumbuzi ni namna gani wanaweza kuondokana na janga hili. Wasomi mbalimbali wameumiza vichwa ni jinsi gani wanaweza kuondokana na janga hili na sio wasomi tu ni tatizo ambalo limekuwa kwa kila mtu aweze kujinusuru na umaskini.
Katika siku ya leo napenda tuangalie hasa kwa undani maana ya umaskini na sababu zinazofanya mtu awe maskini kila kukicha.
Umaskini ni nini?
Kwa tafasri ya harakaharaka Umaskini ni hali ile kitu au mtu anaposhindwa kukidhi na kumudu mahitaji yake kwa muda sitahiki.
Ni maswali mengi unaweza kujiuliza “Je Umaskini ni kukoswa pesa?” au “Je pesa ndio suluhisho la umaskini?” Katika maswali haya unaweza ukawa na majibu ya moja kwa moja kwamba jibu sahihi ni Pesa lakini hebu jaribu kufikiri tena “Je hauwezi kuwa na Pesa na bado ukaendelea kuwa maskini?” Mpendwa msomaji najaribu kukuweka kwenye ulimwengu wa Fikra ujaribu kupambanua wewe kama wewe halafu katika hayo maswali sidhani kama utakoswa jibu.
Kabla sijaenda kuelezea sababu zinazofanya mtu au nchi ikiwemo Tanzania kuendelea kuwa maskini napenda kukuweka wazi kuhusu swala la umaskini. Sio siri kwa mienendo yetu na tabia zetu za kutotambua tunafanya nini na kugandisha  akili zetu zisitake kupanuka na kutaka kila kitu mtelezo waswahili wanavyosema ganda la ndizi tutaendelea kuwa maskini siku hadi siku.
Umaskini sio swala la kukoswa pesa au kuwa na pesa kidogo bali umaskini unaletwa na jinsi gani akili zetu tulivyozilaza hatutaki kushirikisha katika maendeleo maana hata wewe ni shahidi katika umri huo ulio nao sizani kama huna historia ya mtu kumiliki pesa halafu akafirisika na kuishiwa kila kitu hapohapo unaweza kujiuliza ni sababu gani zinamfanya mtu awe na maendeleo halafu ifikie hatua  aishiwe kila kitu. Kumbe tukiangalia uhalisia Umaskini hausababishwi na ukosefu wa pesa ila ni uwezo wa kufikiri na nidhamu katika maendeleo ya mtu Mfano mzuri Mtu anakuwa ana uwezo wa kipato cha laki mbili kwa mwezi lakini nyumba anayoishi amepanga kwa elfu themanini bado anategemea aende shopping  isiyopungua elfu hamsini hapohapo hicho kipato kimulishe na bado hajamtumia mama unafikiri mtu kama huyo baada ya miaka miwili atakuwa na maendeleo gani?
Sababu za Umaskini.
Ndugu, kuna sababu nyingi sana ambazo tunaweza kuziona zinasababisha umaskini ikiwemo vita, ufisadi, maradhi, uvivu na Uzembe, Ukosefu wa Elimu na mambo mengi kadha wa kadha.
Hizo ni baadhi ya sababu zinazochukuliwa kwa tathmini ya umaskini katika nchi n.k “Je unaweza kufikiria sababu hizo ni ukweli zinachangia umaskini hadi kwa mtu binafsi?” jibu najua utakuwa nayo Hebu sasa tuangalie ni sababu nne ambazo mara nyingi zinachangia sana Ongezeko la umaskini barani afrika na hasa kwa wananchi wengi wa Tanzania.
Kwanza “Woga” ni ugonjwa wa maendeleo ambao unahitaji maamuzi yaliyo sahihi kwa mtu binafsi kuweza kujitibu ndugu, sidhani neno  woga linaweza kuwa msamiati kwa mtu anayejua kusoma na kuandika lakini ni ugonjwa mbaya mno katika maendeleo ya mtu na taifa kwa ujumla maana inapofika mahali pa kuchukua maamuzi yaliyo sahihi mtu anaogopa na hili lipo kwa watanzania wengi sana Mfano rahisi ni mtu anapotaka labda kufungua biashara kitu cha kwanza anachowaza ni kwamba  nikipata hasara itakuwaje baada ya kuwaza afungue biashara aboreshe kiasi gani ilia pate soko anawaza kushindwa na kupata hasara na hii imekuwa inarudisha watu nyuma sana na kuendelea kuwa maskini. Ndugu yangu kama una tatizo kama hili nafasi bado unayo chukua maamuzi yaliyo sahihi kwa kile unachofikiria kinaweza kukufanya ufikie ndoto zako ufanye kwa imani yako yote utafanikiwa.
Pili “Ukosefu wa Elimu bora ” Watanzania walio wengi wanashindwa kuendelea sababu ya ukosefu wa Elimu bora ya kujikimu na kuendesha mipango yao madhubuti .Hii pia inaweza kusababishwa na mfumo wa elimu yetu nchini maana sio siri msomaji Mtanzania anaweza kusoma hadi chuo kikuu halafu akaletwa mtaani akaambiwa afanye chochote alichosomea ili kimusaidie katika maisha yake bila kupatiwa ajira (ajiajiri mwenyewe) hawezi.Je unaweza kufikiri tunaelekea wapi? Lakini si hivyo tu kuna kundi kubwa sana ambalo hawawezi hata kujisamamia hata kidogo sababu ya ukosefu wa elimu bora.
Tatu “Uvivu na Uzembe” ni moja ya sababu ambayo inakumba kundi kubwa la watu hasa nchini kwetu ambapo watu wanashindwa kujishughulisha hata kwa kipato kidogo kuweza kujipatia riziki hivyo mtu anabaki na maisha duni na kubaki tegemezi  na maskini kila kukicha.
Nne na Muhimu “Nidhamu ya Pesa” hakuna kitu kinachorudisha na kufanya mtu kuwa na maisha duni na kubaki maskini ni ukosefu wa nidhamu ya pesa mfano mtu yupo tayari kuwa na matumizi ambayo yanazidi kipato  kwa makala zijazo nitaelezea kwa undani ni namna gani mtu anaweza kuwa na nidhamu ya pesa na ikamsaidia katika mafanikio yake na kufikia ndoto zake.